Man United Yalazimishwa Sare ya 1-1 na West Ham, Bao la Mwisho Lamnusuru Sesko
2026-02-11 - 08:08
Manchester United imelazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya West Ham United katika mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa katika dimba la London Stadium, matokeo yaliyokatisha rekodi yao ya ushindi wa mechi nne mfululizo na kuendeleza ukame wa ushindi ugenini dhidi ya Wagonga Nyundo. West Ham walianza kwa kasi na kuonyesha dhamira ya kutafuta mabao mapema, wakilitawala eneo la kiungo huku United wakionekana kushindwa kutengeneza nafasi za wazi kipindi cha kwanza. Kipindi cha pili kilianza kwa presha kutoka kwa wenyeji, na juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 50 baada ya Tomas Soucek kufunga bao la kuongoza akimalizia pasi safi ya Jarrod Bowen, bao lililoamsha shangwe kwa mashabiki wa West Ham. Baada ya bao hilo, United walijaribu kusawazisha kwa kuongeza mashambulizi kupitia safu yao ya ushambuliaji, lakini walikumbana na ukuta imara wa mabeki wa West Ham huku kipa wao akifanya kazi ya ziada kuokoa hatari kadhaa. Dakika zilivyozidi kuyoyoma, ilionekana kama West Ham wangeondoka na ushindi muhimu, lakini dakika za nyongeza zilileta drama. Katika dakika ya 90+6, Benjamin Sesko aliibuka shujaa kwa United baada ya kufunga bao la kusawazisha akipokea pasi ya Bryan Mbeumo na kuihakikishia timu yake pointi moja muhimu. Matokeo hayo yanaifanya Manchester United kuendelea kusota katika dimba la London, wakiwa hawajapata ushindi dhidi ya West Ham ugenini tangu Septemba 19, 2021. FT: West Ham 1-1 Man United 50’ Soucek (A: Bowen) 90+6’ Sesko (A: Mbeumo) SIMBA YATIKISIKA! MO ATOA KAULI NZITO YA KUONDOKA/YANGA YAAPA KUFUZU CAF..#KROSSDONGO