TheTanzaniaTime

Mahakama Yatupilia Mbali Mapingamizi 4 ya Lissu, Lakubali Hoja Kuhusu Kizimba cha Shahidi wa Siri

2026-02-11 - 12:08

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetupilia mbali mapingamizi manne (4) kati ya matano (5) yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, katika kesi ya uhaini inayomkabili. Uamuzi huo umetolewa muda mfupi uliopita katika chumba namba moja cha Mahakama hiyo na kiongozi wa jopo la Majaji wanaosikiliza shauri hilo namba 19605/2025, Jaji Dastan Ndunguru. Mahakama imekubali pingamizi moja pekee lililohusu kizimba kilichojengwa kwa ajili ya mashahidi wa siri, ikieleza kuwa hakikidhi matakwa ya kisheria. Katika hoja yake, Lissu alieleza kuwa kizimba hicho hakiruhusu shahidi wa siri kuonekana na Majaji wanaosikiliza kesi, jambo ambalo linakiuka taratibu za kisheria zinazomtaka shahidi huyo kuonekana na Jaji au Hakimu anayesikiliza shauri husika. Akitoa uamuzi, Mahakama imekubaliana na hoja hizo na kuagiza kizimba hicho kirekebishwe haraka iwezekanavyo, ndani ya siku ya leo, ili kuendana na matakwa ya sheria. Baada ya maamuzi hayo, kesi imeahirishwa hadi kesho Alhamisi, Februari 12, 2026, saa 3:00 asubuhi, ambapo usikilizwaji utaendelea.

Share this post: