Mahakama Kuu Yaiamuru Serikali Kumlipa Bilioni 3.22 Mmiliki wa Jengo Lililobomolewa Mbezi
2026-02-03 - 03:08
Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, imewaamuru aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni pamoja na Naomi Raymond Kwayu kumlipa fidia ya jumla ya Shilingi bilioni 3.22 Johnsen Leonard Mahururu, kufuatia uamuzi wa kubomoa kimakosa jengo lake la makazi katika eneo la Mbezi Africana, jijini Dar es Salaam. Uamuzi huo umetolewa Desemba 30, 2025 na Jaji Sharmillah Sarwatt Kazi, katika kesi ya ardhi Na. 000032646 ya mwaka 2024. Kilichopelekea kesi Mahururu alifungua kesi dhidi ya Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na wadaiwa wengine sita, akipinga hatua ya kubomolewa kwa jengo lake la makazi pamoja na jengo la hoteli mnamo Machi 1, 2024, kwa madai kuwa kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa na Naomi Kwayu. Hata hivyo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama ilibaini kuwa uamuzi wa kubomoa majengo hayo haukuwa halali, kwani Mahururu ndiye mmiliki halali wa kiwanja namba 484 (2196), Block H. Umiliki halali watambuliwa Mahakama ilieleza kuwa Mahururu alinunua kiwanja hicho Januari 31, 2022 kutoka kwa Juma Rajabu Kapungu, ambaye naye alikinunua kutoka Wood Pecker Company Limited mwaka 1997, hivyo kuthibitisha mnyororo halali wa umiliki. Kutokana na hilo, Mahakama imeagiza: Msajili wa Hati kufuta hati ya Naomi Kwayu Mahururu kupewa hati halali ya umiliki Fidia iliyoamriwa Mahakama imeamuru wadaiwa kumlipa Mahururu: Bilioni 3.18 kwa uharibifu wa nyumba ya makazi iliyojengwa kihalali na yenye kibali Milioni 40 kwa gharama nyingine za uharibifu Gharama zote za kesi Fedha hizo zitalipwa na Manispaa ya Kinondoni, aliyekuwa Waziri wa Ardhi Jerry Slaa na Naomi Raymond Kwayu. Hata hivyo, Mahakama imekataa madai ya fidia ya bilioni 16.24 kwa jengo la hoteli, ikisema halikuwa na kibali cha ujenzi.