TheTanzaniaTime

Madai Mazito Yafichuliwa Kati ya Familia Ya Trump na Mwanamfalme – Video

2026-02-02 - 18:29

Ripoti mpya ya uchunguzi iliyochapishwa na gazeti la The Wall Street Journal imeibua mjadala mkubwa wa kisiasa na kiusalama, baada ya kufichua madai ya kuwepo kwa makubaliano ya siri ya kifedha kati ya familia ya Rais wa Marekani, Donald Trump, na shehe mwanamfalme maarufu kama “Spy Sheikh” mwenye ushawishi mkubwa kutoka Abu Dhabi, Falme za Kiarabu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, siku nne tu kabla ya Donald Trump kuapishwa kuingia madarakani, wasaidizi wa karibu wa mwanamfalme huyo wa Abu Dhabi waliingia katika makubaliano ya kununua asilimia 49 ya hisa katika mradi wa sarafu-fiche (cryptocurrency) unaohusishwa na familia ya Trump. Thamani ya dili hilo inatajwa kufikia dola milioni 500 za Marekani takribani shilingi Trilioni 1.29. Mradi huo wa kidijitali, unaojulikana kama World Liberty Financial, unadaiwa kuhusisha watu wa karibu na familia ya Trump pamoja na washirika wa kibiashara. Ripoti inaeleza kuwa takribani dola milioni 250 zililipwa mara moja, ambapo dola milioni 187 zilienda kwenye taasisi zinazohusishwa na familia ya Trump, huku kiasi cha dola milioni 31 zikielekezwa kwa taasisi zinazohusishwa na familia ya Steve Witkoff, afisa mwandamizi wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati. Kilichozua maswali makubwa ni kwamba makubaliano hayo hayakutangazwa hadharani, na yalibainika miezi kadhaa baadaye kupitia uchunguzi wa nyaraka za ndani na vyanzo vya karibu na mazungumzo hayo. Wachambuzi wanasema muda wa kufanyika kwa dili hilo ni wa kutia shaka, hasa ikizingatiwa kuwa baada ya Rais Trump kuingia madarakani, kulikuwa na mabadiliko ya sera kati ya Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu, ikiwemo masuala yanayohusiana na teknolojia nyeti za akili bandia. Hata hivyo, wawakilishi wa familia ya Trump wamekanusha madai ya ukiukwaji wa maadili, wakisisitiza kuwa makubaliano hayo yalikuwa ni uwekezaji wa kibiashara halali, na kwamba rais hakuhusika moja kwa moja katika uendeshaji wa mradi huo. Kadri mjadala unavyoendelea, wabunge na wataalamu wa maadili nchini Marekani wanataka uchunguzi zaidi, wakisema sakata hili linaibua maswali mazito kuhusu uwazi, mgongano wa maslahi, na ushawishi wa fedha za kigeni katika uongozi wa kisiasa wa Marekani, chini ya utawala wa Raid Donald Trump.

Share this post: