TheTanzaniaTime

Lissu Alalamikia Kutopatiwa Chakula, Kesi Yaahirishwa Kwa Muda

2026-02-12 - 12:59

Dar es Salaam – Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, imeahirishwa kwa muda wa dakika 15 baada ya mshtakiwa huyo kulalamikia kutopatiwa chakula cha mchana akiwa mahabusu. Awali, Mahakama ilikuwa imeahirisha shauri hilo kwa takribani saa mbili ili kutoa nafasi kwa watu waliokuwepo mahakamani kupata chakula cha mchana, sambamba na kuruhusu upande wa Jamhuri kujiandaa kumleta shahidi mwingine kufuatia shahidi wa awali, aliyetambulika kama P5, kukamilisha ushahidi wake. Hata hivyo, baada ya Mahakama kurejea kuendelea na usikilizwaji wa kesi, Lissu alieleza kuwa hakupatiwa chakula na Maafisa wa Jeshi la Magereza licha ya kuwa na haki hiyo. Alifafanua kuwa kwa mujibu wa taratibu za magereza, mahabusu hujigharamia chakula, na yeye ana fedha zake binafsi zinazoshikiliwa na mamlaka ya Magereza, jambo lililomshangaza kushindwa kupatiwa huduma hiyo. Pamoja na hali hiyo, Lissu alisisitiza kuwa yuko tayari kuendelea na usikilizwaji wa kesi bila kula, huku Mahakama ikiahirisha kwa muda mfupi ili suala hilo kushughulikiwa. Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu, huku ikivuta hisia za wengi kutokana na uzito wake wa kisiasa na kisheria.

Share this post: