TheTanzaniaTime

Lishe ya Keto Yatajwa Kupunguza Msongo wa Mawazo (depression)

2026-02-21 - 00:06

Ulaji wa lishe yenye mafuta mengi na wanga kidogo, maarufu kama lishe ya ketogenic (keto), unaweza kusaidia kupunguza dalili za msongo wa mawazo (depression), kwa mujibu wa tafiti za hivi karibuni. Msongo wa mawazo ni miongoni mwa matatizo ya afya ya akili yanayoathiri watu wengi duniani. Nchini Uingereza, takwimu zinaonyesha kuwa takribani mtu mmoja kati ya watano amewahi kukumbwa na hali hiyo katika maisha yake. Hata hivyo, kwa karibu theluthi moja ya wagonjwa, dawa za kupunguza msongo wa mawazo haziondoi kikamilifu dalili hali inayojulikana kama treatment-resistant depression. Watafiti sasa wanaamini kuwa mabadiliko ya lishe yanaweza kuwa nyongeza muhimu katika matibabu. Lishe ya Keto ni Nini? Lishe ya keto ni mpango wa ulaji unaosisitiza mafuta mengi, protini ya wastani, na wanga kidogo sana (chini ya gramu 30 kwa siku katika tafiti nyingi). Lishe hii husababisha mwili kuingia katika hali inayoitwa ketosis, ambapo badala ya kutumia wanga kama chanzo cha nishati, mwili hutumia mafuta. Wataalamu wanaamini kuwa mabadiliko haya ya kimetaboliki yanaweza kupunguza uvimbe (inflammation) kwenye ubongo jambo linalohusishwa na msongo wa mawazo na matatizo mengine ya afya ya akili. Kwa sasa, lishe ya keto tayari hutumika rasmi katika matibabu ya kifafa, na tafiti mpya zinaanza kuchunguza matumizi yake kwa magonjwa mengine ya akili kama bipolar na skizofrenia. Watafiti kutoka University of Oxford walifanya utafiti uliowahusisha watu 88 waliokuwa na msongo wa mawazo ambao haukuwa umeitikia vyema dawa za kawaida. Washiriki waligawanywa katika makundi mawili: Kundi la keto: Lilipewa milo maalum na vitafunwa vyenye chini ya gramu 30 za wanga kwa siku. Kundi lisilo la keto: Liliendelea kula kawaida, lakini lilipewa ushauri wa kuboresha lishe kama kubadilisha mafuta yasiyofaa na kula matunda na mboga zaidi. Makundi yote yaliendelea kutumia dawa zao za kawaida. Baada ya wiki sita, wale waliokuwa kwenye lishe ya keto walionyesha kupungua kwa kiwango kikubwa cha dalili za msongo wa mawazo ikilinganishwa na kundi la kawaida. Aidha, utafiti wa mwaka 2025 uliowahusisha wanafunzi wa vyuo vikuu ulibaini kuwa lishe ya keto ilipunguza dalili za msongo wa mawazo kwa hadi asilimia 70. Ingawa lishe peke yake si tiba kamili ya msongo wa mawazo, tafiti hizi zinaongeza ushahidi kuwa chakula tunachokula kinaweza kuwa na athari kwa afya ya akili. Kwa yeyote anayefikiria kuanza lishe ya keto, ni muhimu kushauriana na mtaalamu wa afya kabla ya kufanya mabadiliko makubwa ya lishe, hasa kama tayari anatumia dawa au ana hali nyingine za kiafya.

Share this post: