Kesi ya Lissu Kusikilizwa Siku 20 Mfululizo Mahakama Kuu – Video
2026-02-09 - 07:28
Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, inatarajiwa kuendelea leo katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, huku upande wa mashtaka ukitarajia kujibu hoja za kisheria zilizowasilishwa na utetezi kupinga uhalali wa matumizi ya mashahidi fiche wa Jamhuri. Usikilizwaji wa shauri hilo umewekwa kufanyika kwa siku 20 mfululizo za kazi kuanzia leo Jumatatu, Februari 9, 2026 hadi Machi 6, 2026, hatua inayotarajiwa kuharakisha mwenendo wa kesi hiyo inayovuta hisia za wananchi na wadau wa siasa pamoja na sheria nchini. Katika pingamizi lake, Lissu anapinga uamuzi wa upande wa mashtaka kutegemea mashahidi ambao hawatafichua utambulisho wao hadharani, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri haki ya mshtakiwa kupata usikilizwaji wa haki na wa wazi. Upande wa Jamhuri kwa upande wake unatarajiwa kuwasilisha majibu ya kisheria kutetea matumizi ya mashahidi hao, ukidai kuwa ni muhimu kwa maslahi ya usalama na ulinzi wa mashahidi husika. Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, alitoa maneno na kauli za uchochezi zenye lengo la kushawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na majaji James Karayemaha pamoja na Ferdinand Kiwonde. Kwa sasa, shauri hilo liko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka, huku matarajio yakiwa ni kuona mwelekeo wa kesi hiyo utachukua sura gani baada ya maamuzi ya mahakama kuhusu pingamizi la mashahidi fiche. Kesi ya Lissu imeendelea kuwa gumzo kubwa kisiasa na kisheria, huku wadau wengi wakifuatilia kwa karibu mwenendo wake kutokana na uzito wa mashtaka yanayomkabili mwanasiasa huyo mkongwe.