Katambi Aanza Kazi Rasmi, Apongeza Jeshi la Polisi
2026-01-28 - 15:36
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amesema Nchi ya Tanzania iko salama huku akigusia uimara wa Jeshi la Polisi la Tanzania ambalo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama limeweza kuiweka Nchi salama tangu nchi ipate uhuru. Ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kwanza ya kutembelea Makao Makuu ya Jeshi, jijini Dodoma baada ya kuteuliwa kuongoza wizara hiyo ambapo aliambata na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahomud na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Miriam Mmbaga. Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahomud amesema kuwa umoja na mshikamano ndani ya Jeshi hilo pamoja na ushirikiano wake na wananchi umechangia kwa kiasi kikubwa kudumisha amani na utulivu nchini, hali inayowawezesha Watanzania kuendelea kufurahia matunda ya uhuru wao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kukuza uchumi wa Taifa.