Kamishna Mwenda: Idara ya Forodha ni Nguzo ya Usalama na Ulinzi wa Taifa
2026-01-25 - 21:09
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa licha ya kuwezesha biashara imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kulinda mipaka na afya za watanzania kwa kuzuia bidhaa zisizofaa kuingia nchini. Kamshna Mwenda ameyasema hayo wakati wa bonanza la michezo mbalimbali lililofanyika katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam leo Januari 25.2026 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Forodha Duniani ambayo huadhimishwa Januari 26 kila mwaka. Kamishna Mkuu Mwenda amesema mchango wa Idara ya Forodha kwa usalama wa watanzania ni mkubwa. Amesema wanapofanya kazi ya ukaguzi wa mizigo wamekuwa wakiwezesha bidhaa zisizostahili kutokuingia nchini na kuikinga nchi na athari zinazoweza kusababishwa na matumizi ya bidhaa zisizofaa. Bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu ambapo TRA iliibuka kidedea dhidi ya Mawakala wa Forodha baada ya kufunga bao 2 kwa 0 huku kukiwa na michezo ya kuvuta kamba, kukimbia kwa magunia na kukimbiza kuku.