Kamisheni ya Utalii Zanzibar Yatoa Mwongozo Maalum Kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani
2026-02-12 - 12:39
Zanzibar – Kamisheni ya Utalii Zanzibar imewataka watalii, wafanyabiashara pamoja na wadau wote wa sekta ya utalii visiwani humo kuheshimu maadili ya dini na utamaduni wa jamii ya Zanzibar katika kipindi hiki cha kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kupitia mwongozo huo, Kamisheni imesisitiza kuwa migahawa na sehemu za chakula zilizo nje ya hoteli zinatakiwa kufungwa wakati wa mchana hadi jua linapozama kwa ajili ya futari (iftar). Aidha, imepiga marufuku kula, kunywa au kuvuta sigara hadharani wakati wa mchana katika kipindi chote cha Ramadhani. Vilevile, wageni na wakazi wametakiwa kuvaa mavazi yenye staha katika maeneo ya umma, huku mavazi yanayoonesha sehemu kubwa za mwili yakipigwa marufuku. Kamisheni imewataka pia wadau wa utalii kuwajulisha na kuwakumbusha wafanyakazi wao kuhusu mwongozo huo, pamoja na kubandika matangazo ya tahadhari katika maeneo ya biashara na huduma ili kuhakikisha kila mmoja anazingatia taratibu hizo. Hatua hiyo inalenga kudumisha heshima, utulivu na maadili ya kijamii wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambao ni muhimu kwa waumini wa dini ya Kiislamu.