TheTanzaniaTime

Fahamu Madhara ya Kuendesha Gari Taa ya Mafuta Ikiwa Inawaka

2026-02-12 - 06:09

Madereva wengi wana tabia ya kupuuza taa ya mafuta pale inapowaka kwenye dashboard ya gari, wakiamini bado wanaweza kusafiri umbali mrefu kabla ya tanki kuisha kabisa. Wengine husema, “bado naweza kufika kituo kijacho”, au “nitaweka baadaye.” Hata hivyo, wataalamu wa magari wanaonya kuwa kuendesha gari kwa muda mrefu huku taa ya mafuta ikiwa imewaka kunaweza kusababisha madhara makubwa kiusalama na kiufundi, na wakati mwingine kuigharimu fedha nyingi zaidi kuliko kujaza mafuta mapema. Ifuatayo ni baadhi ya madhara yanayoweza kujitokeza: 1.Gari kuzimika ghafla barabarani Taa ya mafuta inapowaka, mara nyingi hubaki kiasi kidogo sana cha mafuta kinachotosha kwa kilomita chache tu. Endapo mafuta yataisha ukiwa safarini, gari linaweza kuzimika ghafla bila onyo lolote. Hali hii inaweza kuwa hatari zaidi ukiwa: barabara kuu kwenye foleni au usiku Kuzimika kwa ghafla kunaweza kusababisha ajali au usumbufu mkubwa kwa watumiaji wengine wa barabara. 2.Uharibifu wa pampu ya mafuta (fuel pump) Watu wengi hawajui kuwa pampu ya mafuta hupozwa na kulainishwa na mafuta yenyewe. Tanki linapokuwa karibu tupu, pampu hulazimika kufanya kazi bila mafuta ya kutosha. Matokeo yake: pampu hupata joto kupita kiasi huisha nguvu mapema au kuungua kabisa Gharama ya kubadilisha pampu ya mafuta inaweza kuwa kubwa sana kulingana na aina ya gari. 3.Uchafu kuingia kwenye mfumo wa mafuta Chini ya tanki la mafuta mara nyingi hukusanyika masalia kama: kutu vumbi uchafu wa mafuta Unapokuwa na mafuta kidogo, pampu huvuta uchafu huo moja kwa moja na kuuingiza kwenye mfumo wa mafuta. Hali hii inaweza kusababisha: kuziba kwa fuel filter kuharibika kwa injectors gari kuchechemea au kupoteza nguvu ya engine 4.Kuongezeka kwa matumizi ya mafuta Ingawa baadhi ya madereva hudhani wanaokoa kwa kuchelewesha kujaza mafuta, ukweli ni kwamba engine inapofanya kazi katika hali ya mafuta kidogo, mwako hauwi mzuri na matumizi yanaweza kuongezeka. Hivyo, badala ya kuokoa, unajikuta unatumia zaidi. 5.Msongo wa mawazo wakati wa safari Mbali na uharibifu wa kiufundi, kuendesha gari taa ikiwa imewaka huleta hofu na presha isiyo ya lazima. Dereva hulazimika kutafuta kituo cha mafuta kwa haraka au kuendesha kwa wasiwasi akihofia gari kuzima muda wowote. Safari inakuwa ya mashaka badala ya utulivu. Kwa kifupi, taa ya mafuta ni onyo muhimu, si mapambo ya dashboard. Kupuuza ishara hiyo kunaweza kusababisha hasara kubwa ya fedha na kuhatarisha usalama wako. Wataalamu wanashauri kujaza mafuta mapema, angalau tanki linapofika robo (1⁄4), ili kuepuka matatizo yasiyo ya lazima.

Share this post: