El Mencho Afariki, CJNG Washambulia Majimbo Kadhaa kwa Kulipiza Kisasi
2026-02-23 - 16:27
Wanachama wa Kundi la Kihalifu la Wauza Dawa za Kulevya, Jalisco New Generation (CJNG), moja ya makundi yanayoogopwa zaidi nchini Mexico, wameanzisha wimbi la vurugu katika majimbo 20 ya Mexico. Wamechoma moto biashara mbalimbali na kuweka vizuizi vya barabarani vinavyowaka moto ikiwa ni kulipiza kisasi kufuatia kuuawa kwa kiongozi wao, Nemesio Oseguera Cervantes almaarufu El Mencho, aliyefariki akiwa kizuizini siku ya Jumapili muda mfupi baada ya kukamatwa na vikosi maalum vya Mexico. El Mencho, aliyekuwa mtu anayetafutwa zaidi nchini Mexico, alijeruhiwa vibaya katika mapambano ya risasi kati ya walinzi wake na makomandoo wa kijeshi waliotumwa kumkamata. Alifariki dunia wakati jeshi lilipokuwa likimsafirisha kutoka mji wa Tapalpa, katika Jimbo la Jalisco, kuelekea mji mkuu, Mexico City. Takribani walinzi sita wa usalama wa El Mencho pia waliuawa katika operesheni hiyo, huku wanajeshi watatu wa Mexico wakijeruhiwa, kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi. Kadiri taarifa za kifo cha El Mencho zilivyoenea, wanachama wa kundi lake walianzisha mashambulizi katika miji na majiji mengi ambako CJNG inafanya shughuli zake. Katika baadhi ya miji, walizuia barabara kwa kutupa miiba na misumari barabarani; katika mingine, waliteka mabasi na magari mengine kisha kuyachoma moto katikati ya barabara. Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.