Donald Trump Ahoji Kwa nini Iran Bado Haijakubali Masharti, Atoa Siku 10 – Video
2026-02-23 - 07:38
Mjumbe maalum wa Marekani, Steve Witkoff Rais wa Marekani Donald Trump amehoji kwa nini Iran bado haijakubali masharti ya makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia, licha ya kuongezeka kwa nguvu za kijeshi za Marekani katika Mashariki ya Kati, kwa mujibu wa mjumbe wake maalum, Steve Witkoff. Akizungumza na Fox News Jumamosi, Witkoff alisema Trump anataka majibu kuhusu kusitasita kwa Tehran, hasa baada ya kuonya uwezekano wa mashambulizi ya kijeshi endapo makubaliano hayatapatikana ndani ya muda mfupi. Marekani na baadhi ya washirika wake wa Ulaya wanaishuku Iran kuwa inakaribia uwezo wa kutengeneza silaha ya nyuklia mjadala ambao Tehran imekuwa ikikanusha mara kwa mara. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema bado kuna dirisha la suluhu ya kidiplomasia kwa misii kwa pande zote. Ameongeza kuwa Tehran inaandaa rasimu ya makubaliano itakayowasilishwa kwa upande wa Marekani, ikilenga kuweka njia ya kupunguza mvutano na kurudisha uaminifu. Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran yalifanyika Geneva, Uswisi, Februari 17, yakipatanishwa na Badr Albusaidi wa Oman. Raundi nyingine imetangazwa kufanyika wiki hii, hatua ambayo inaweza kuweka mwelekeo wa mustakabali wa mazungumzo. Hivi karibuni, Marekani imeongeza uwepo wake wa kijeshi karibu na Iran. Meli kubwa ya kivita ya USS Gerald R. Ford na USS Abraham Lincoln zimeripotiwa kuelekea ukanda huo, zikiandamana na manowari, meli za kivita na ndege za kijeshi. Hatua hii inalenga kuongeza shinikizo kwa Tehran huku ikitoa onyo la kile ambacho Washington inaliita “chaguo la kijeshi” endapo diplomasia itakwama. Trump amesema dunia inaweza kufahamu ndani ya siku 10 zijazo iwapo makubaliano yatafikiwa au hatua za kijeshi zitachukuliwa kauli inayoongeza hisia za dharura kwenye mchakato wa mazungumzo. Wakati mvutano wa kimataifa ukiendelea, ndani ya Iran kumekuwa na ripoti za maandamano katika vyuo vikuu kadhaa. Uhamasishaji huo wa wanafunzi unaashiria kuongezeka kwa presha ya ndani, ambayo inaweza kuwa na athari katika mkao wa serikali mezani kwenye mazungumzo ikiwemo kusukuma msimamo mkali zaidi au kuongeza nia ya kupata makubaliano ya haraka.