Dkt. Mwigulu Kuzindua Miundombinu ya Kisasa ya Utalii Hifadhi ya Nyerere
2026-02-11 - 06:59
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Februari 11, 2026, ameelekea katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa ajili ya kuzindua na kukabidhi rasmi miundombinu mbalimbali ya utalii inayolenga kuimarisha sekta hiyo pamoja na kuongeza mapato ya taifa. Katika ziara hiyo, Dkt. Mwigulu anatarajiwa kufungua na kukagua miradi ikiwemo barabara za ndani ya hifadhi, malazi ya watalii, vituo vya huduma kwa wageni pamoja na maboresho ya miundombinu ya usafiri na mawasiliano. Akizungumza kabla ya hafla hiyo, viongozi wa TANAPA wamesema maboresho hayo yataongeza idadi ya watalii, kuboresha uzoefu wao na kufungua fursa zaidi za ajira kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo. Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya utalii kama moja ya nguzo muhimu za uchumi, huku Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ikitajwa kuwa miongoni mwa vivutio vikubwa barani Afrika kutokana na wanyamapori na mandhari yake ya kipekee. Uzinduzi huo unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wadau wa utalii pamoja na wananchi wa maeneo jirani.