Dkt. Lazaro Komba Ateuliwa Mgombea CCM Jimbo la Peramiho
2026-01-26 - 06:57
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imemteua Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Dkt. Lazaro Komba, kuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Peramiho, mkoani Ruvuma. Uamuzi huo uliotangazwa, Januari 25, 2026, na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi umekata mzizi wa fitina baada ya Dkt. Komba aliyekuwa mshindi wa tano katika kura za maoni kuaminiwa na chama huku Victor Mhagama aliyekuwa anaongoza akiaachwa. Uamuzi huo ulifanyika baada ya kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika visiwani Zanzibar na kuongoza na Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Samia Suluhu Hassan. Victor Mhagama, ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Marehemu Jenista Mhagama, aliongoza kura za maoni kwa kupata kura 3,040, akifuatiwa na Getrude Haule (2,913). Dkt. Komba alipata kura 213 pekee. Hata hivyo, mchakato huo uligubikwa na tuhuma za rushwa na lugha zisizofaa, hali iliyopelekea TAKUKURU kuwahoji baadhi ya watia nia akiwemo Victor. “Kwa kuzingatia mamlaka iliyopewa chini ya Ibara ya 105 (7)(f) ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la Julai 2025, Kamati Kuu imefanya uteuzi Dk Lazaro Komba kuwa mgombea wa CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Peramiho, lililopo Wilaya ya Songea Vijijini,” alisema.