TheTanzaniaTime

Canon Europe Yaendeleza Ushirikiano na Infocus Studio Kupitia Ziara Rasmi

2026-02-10 - 09:39

Infocus Studio imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na Canon kupitia ziara rasmi ya uongozi kutoka Canon Europe. Ziara hiyo iliongozwa na Bw. Ozgur Kocademir, Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko – DRBG, Canon Europe, kwa lengo la kuendeleza mahusiano ya kimkakati, kutathmini hatua zilizofikiwa na Infocus Studio, pamoja na kuoanisha mipango ya pamoja kwa mwaka 2026 na kuendelea. Aidha katika ziara hiyo, pande zote mbili zilijadili kwa kina ukuaji wa Afrika Mashariki katika utengenezaji wa maudhui na jinsi ushirikiano wa aina hii unavyoweza kuvunja mipaka, kupanua fursa, na kuwezesha maudhui kutoka Afrika Mashariki kufika Afrika nzima na hata dunia nzima. Ziara hiyo pia iligusia uwekezaji mpya wa Infocus Studio katika vifaa vya uzalishaji, ikiwemo kuongeza uwezo wa kampuni kupitia ununuzi wa kamera mpya za Canon C50 (toleo la 2026) zenye uwezo wa kurekodi hadi 7K Open Gate pamoja na teknolojia ya kisasa ya Akili Bandia (AI) kwa ufanisi zaidi katika mazingira ya uzalishaji wa maudhui ya kisasa. Uwekezaji huu unalenga kuongeza ushindani wa Infocus Studio ndani ya nchi na kimataifa, sambamba na mahitaji mapya ya soko la maudhui. Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Ozgur Kocademir alisisitiza kuwa ushirikiano wa Canon na Infocus Studio unaendelea vizuri na kwamba Canon inalenga kuukuza zaidi uhusiano huo kwa mwaka 2026, ikivutiwa na ari na uwezo wa Infocus kufanya mengi zaidi katika tasnia. “We can make more out of your experiences, because this is not one way,it’s two way. This is very big,” alisema Bw. Ozgur Kocademir. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Infocus Studio, Bw. Joshua Moshi, alisema kuwa ushirikiano huu kati ya Canon na Infocus umeendelea kuwapa nguvu kama taasisi inayojikita katika kubadilisha namna utengenezaji wa maudhui unavyochukuliwa nchini na kwamba lengo ni kuhakikisha wanaweza kwenda na kasi ya soko la kidunia na wakati huo huo kuweza kusaidia kampuni nyingine tanzu za kiTanzania. “I’m always looking for a way to actually take what we are doing here and rub it off to other Tanzanians,” alisema Bw. Joshua Moshi, akisisitiza umuhimu wa kushirikisha maarifa, viwango, na weledi ili manufaa ya kazi ya Infocus yaguse Watanzania wengi zaidi. Akiendelea, aliongeza kuwa kuwekeza kwenye vifaa vya kisasa si suala la “muonekano” pekee, bali ni sehemu ya msingi ya namna Infocus inavyojenga ubora na uimara wa kazi zao kwa muda mrefu. Hatua hii inaashiria ukuaji wa mahusiano kati ya Canon na Infocus Studio na inaonesha jinsi ushirikiano imara kati ya kampuni za ndani na viongozi wa teknolojia duniani unavyoweza kuchochea maendeleo katika tasnia ya ubunifu. Infocus Studio na Canon sasa wanatazamia utekelezaji wa mipango ya pamoja ya 2026 na kuendelea, kwa lengo la kuongeza ubora wa maudhui, kuongeza ufanisi wa uzalishaji, na kupanua wigo wa kazi ndani na nje ya Tanzania. Infocus Studio ni kampuni ya Kitanzania inayojihusisha na utengenezaji wa maudhui, uzalishaji wa video, na kurusha matukio mubashara (live streaming). Kampuni imefanikiwa kufanya kazi na taasisi na chapa mbalimbali, ikiwemo CRDB, World Bank, Vodacom, Serikali ya Tanzania na wizara mbalimbali, pamoja na kushiriki katika uzalishaji na urushaji wa matukio makubwa ya burudani na maudhui ya kimataifa, ikiwemo miradi ya wasanii wakubwa barani Afrika kama vile Tamasha la Castle lite pamoja na ujio wa raia wa kigeni wanawasili kuitangaza Tanzania kama kivutio cha utaili kama vile Braydon Bent.

Share this post: