CAF Yatoa Adhabu kwa Morocco na Senegal Baada ya Vurugu za Fainali
2026-01-29 - 10:34
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza rasmi adhabu dhidi ya timu za taifa za Morocco na Senegal kufuatia vurugu na vitendo visivyo vya kispoti vilivyoshuhudiwa wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2026. Tangazo hilo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka barani Afrika, huku kila upande ukiamini kuwa mpinzani wake ndiye aliyekuwa na makosa makubwa zaidi katika mchezo huo uliogubikwa na utata, kusimama kwa muda na malalamiko dhidi ya maamuzi ya waamuzi. Kwa mujibu wa uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya CAF, kocha wa Senegal, Pape Thiaw, amepigwa marufuku ya michezo mitano ya mashindano ya CAF na kutozwa faini ya dola 100,000 za Marekani, kutokana na mwenendo usio wa kispoti baada ya kuwaagiza wachezaji wake waondoke uwanjani kupinga uamuzi wa refa wakati wa fainali hiyo dhidi ya Morocco. Aidha, Shirikisho la Soka la Senegal limeamriwa kulipa faini ya dola 615,000, ikitajwa kuwa ni kutokana na mwenendo wa timu pamoja na vitendo vya mashabiki wake. Wachezaji Iliman Ndiaye na Ismaila Sarr pia wamesimamishwa kwa michezo miwili ya mashindano ya CAF kila mmoja, kwa tabia ya kutozingatia taratibu na kumkosea heshima mwamuzi wa mchezo. Kocha wa Senegal, Pape Thiaw Hata hivyo, CAF ilitupilia mbali ombi la Morocco lililokuwa likiitaka matokeo ya mechi hiyo kubatilishwa, baada ya wachezaji wa Senegal kuondoka uwanjani kwa takribani dakika 14. Kamati ya Nidhamu ilisema kuwa, licha ya tukio hilo, hakukuwa na msingi wa kisheria wa kubatilisha matokeo ya mchezo. Upande wa wenyeji Morocco nao haukuachwa salama. CAF imeitoza faini ya jumla ya dola 315,000, ikieleza kuwa adhabu hiyo inatokana na mwenendo wa wavulana wa mipira (ball boys), tabia za wachezaji na maofisa wa timu katika eneo la VAR, pamoja na matumizi ya mwangaza wa leza kutoka kwa mashabiki wakati wa mchezo. Vilevile, kapteni wa Morocco, Achraf Hakimi, amesimamishwa kwa michezo miwili ya CAF, adhabu ambayo mchezo mmoja umesimamishwa kwa kipindi cha mwaka mmoja. Ismael Saibari naye amefungiwa michezo mitatu ya CAF, baada ya wote kuhusishwa na kitendo kisicho cha kispoti cha kujaribu kuondoa taulo ya kipa wa Senegal, Edouard Mendy, wakati mvua ikiendelea kunyesha mjini Rabat. Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa mchezo baada ya goli la Senegal kubatilishwa, hali iliyosababisha maandamano ya wachezaji wao na hatimaye kuondoka uwanjani kwa amri ya kocha Thiaw. Dakika chache baadaye, Morocco walipata penati, ambayo mshambuliaji Brahim Diaz aliikosa. CAF imesisitiza kuwa adhabu hizo zinalenga kulinda heshima ya mchezo wa soka, kuhakikisha nidhamu inazingatiwa, na kutoa funzo kwa timu, wachezaji na mashabiki kabla ya mashindano yajayo ya kimataifa barani Afrika.