BRELA Kuimarisha Urasimishaji na Mifumo ya Kidijitali
2026-03-05 - 17:48
Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga ameitaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuongeza kasi ya urasimishaji wa biashara na kuimarisha mifumo ya kidijitali ili kuchochea ufanisi na ukuaji wa uchumi, akisisitiza kuwa taasisi hiyo ni lango kuu la uwekezaji nchini. Akifungua Baraza la Wafanyakazi Machi 4, 2026, Waziri Kapinga alihimiza uwekezaji katika rasilimali watu kupitia mafunzo, stahiki na uadilifu kazini. Alieleza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya biashara zipo sekta isiyo rasmi, hivyo BRELA ina jukumu la kuzirasimisha ili ziweze kunufaika na mikopo, masoko na ulinzi wa kisheria. Aidha, ameagiza kuhuishwa kwa mifumo ya TEHAMA iwe rafiki, salama na inayopunguza muda na gharama kwa wateja, pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mrejesho wa haraka ili kuboresha huduma. Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi huku akiitaka BRELA kuhamia kwenye mfumo wa uwezeshaji badala ya udhibiti pekee. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Bw. Godfrey Nyaisa amesema BRELA imevuka lengo la mapato kwa asilimia 105 katika nusu mwaka wa 2025/26 na kuwasilisha Sh bilioni 3.1 kwa Msajili wa Hazina. Ameeleza kuwa Mpango Mkakati wa 2026–2031 utaboresha huduma za usajili, miundombinu na maslahi ya watumishi ili kuongeza tija.