Balozi wa Iran: Kenya Haina Kituo cha Kijeshi cha Marekani cha Kushambulia Iran
2026-03-03 - 00:18
Balozi wa Iran nchini Kenya, Dkt. Ali Gholampour Balozi wa Iran nchini Kenya, Dkt. Ali Gholampour, amesema Kenya haina kituo cha kijeshi cha Marekani chenye uwezo wa kushambulia Iran, hivyo hakuna sababu ya taifa hilo la Afrika Mashariki kuwa shabaha ya mashambulizi ya Iran. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi, balozi huyo alisisitiza kuwa Kenya haina kikosi cha kijeshi cha Marekani chenye umuhimu wa kimkakati wa kuhalalisha shambulizi. “Nchi hii haina kituo cha kijeshi cha Marekani chenye ukubwa wa kushambulia Iran,” alisema. Kauli hiyo inakuja wakati Iran ikiendelea na mashambulizi katika ukanda wa Mashariki ya Kati, ikisema ni hatua za kulipiza kisasi kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel yaliyomuua Kiongozi Mkuu wake, Ali Khamenei, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa serikali. Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, makombora ya Iran yameripotiwa kulenga nchi kadhaa zikiwemo United Arab Emirates, Qatar, Saudi Arabia, Iraq, Oman, Kuwait, Jordan na Bahrain. Hali ya taharuki imeongezeka tangu mashambulizi ya Jumamosi yaliyoelezwa kuhusisha Marekani na Israel. Balozi Gholampour alielezea mashambulizi hayo kama “ukiukaji wa amani na utulivu wa kimataifa,” akisema Iran ina haki ya kujilinda kama taifa huru. Pia alionya kuwa Marekani na Israel zitawajibika kwa athari za hatua zao. “Umefungua mlango ambao huwezi kuufunga,” alionya. Aidha, aliutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka kuitisha kukomeshwa kwa ongezeko la mashambulizi. Kufuatia mashambulizi hayo, Iran, Iraq, Israel, Syria, Kuwait na Falme za Kiarabu zilitangaza kufungwa kwa muda kwa anga zao kama tahadhari ya kiusalama. Kauli ya balozi huyo inalenga kutuliza hofu miongoni mwa wananchi wa Kenya huku mvutano wa kimataifa ukiendelea kuongezeka katika ukanda wa Mashariki ya Kati. Stori na Elvan Stambuli, Global Digital