TheTanzaniaTime

Balozi Na Bodi Ya Utalii Uganda Watembelea Kituo Cha Polisi Utalii Arusha

2026-02-04 - 08:28

Balozi wa Uganda Nchini Tanzania katika Ofisi ndogo za Arusha, Anne Katusiime leo Februari 03, 2026 ameongoza ujumbe wa Bodi ya Utalii wa Nchi hiyo kutembelea kituo cha Polisi Utalii na Diplomasia Mkoani Arusha kwa lengo la kujifunza namna ambavyo kituo hicho kinahudumia Watalii. Akizungumza baada ya kumaliza ziara hiyo kwa niaba ya Balozi, Afisa Mfawidhi Mdhibiti wa ubora kutoka Bodi ya Utalii Nchini Uganda, Bi. Angela Nyesiga ameshukuru namna ambavyo wamepata ushirikiano muda wote walipokua kituoni hapo na kueleza kuwa ujuzi walioupata kituoni hapo watautumia katika kuimarisha sekta ya utalii nchini kwao. Aidha, amesema kuwa uhalifu hauna mipaka hivyo ni muhimu kwa Nchi hizo mbili kuimarisha mahusiano kwa maslahi mapana ya kiuchumi hususani katika sekta ya utalii na kuhakikisha uhalifu unakomeshwa katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Polisi Utalii na Diplomasia Mkoa wa Arusha , Mrakibu wa Polisi SP Waziri Tenga amesema pamoja na mambo mengine, ujumbe huo umepata fursa ya kujifunza namna ambavyo wanatoa huduma kwa Watalii na Wanadiplomasia sambamba na ambavyo wanashirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii hapa Nchini. Katika hatua nyingine Bi. Hope Tumaini Soyala ambaye aliibuka mshindi tuzo za ‘’Serengeti Awards 2025’’ katika kipengele cha Muongoza Utalii bora wa Kike, alifika katika Kituo hicho kwa ajili ya kutoa shukrani zake kwa Jeshi la Polisi kwa ushirikiano aliokuwa anaupata katika utekelezaji wa majukumu yake ambao ulichangia ushindi wake.

Share this post: