Arsenal Yatinga Fainali Kwa Jasho, Yaitupa Nje Chelsea Kwa Bao la Dakika za Mwisho
2026-02-04 - 07:38
Arsenal imefanikiwa kutinga fainali ya Carabao Cup baada ya kuibwaga Chelsea kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali, na kufuzu kwa jumla ya mabao 4-2. Ingawa mchezo huo haukuwa wa kuvutia sana kwa mashabiki wa soka, wafuasi wa Arsenal hawakujali kabisa ubora wa burudani kilichowahusu ni ushindi na tiketi ya kwenda Wembley. Baada ya kuumizwa na maumivu ya kupoteza nusu fainali nne mfululizo, safari hii “The Gunners” walifanikiwa kuvuka kikwazo hicho licha ya mchezo kuwa wa taratibu na nafasi chache sana za kufunga. Kwa kushangaza, kila timu ilipiga mashuti mawili tu yaliyolenga lango katika dakika 90+ za mchezo, jambo lililoonesha namna mechi ilivyokuwa ya tahadhari na ukosefu wa makali. Bao pekee la mchezo lilifungwa na Kai Havertz dakika za mwisho kabisa (97’), akaiandikia Arsenal ushindi muhimu kabla ya refa kupuliza kipenga cha mwisho. Ushindi huo umeifanya Arsenal kurejea Wembley Park kwa mara nyingine tena kucheza fainali, ambapo watakutana na mshindi kati ya Manchester City au Newcastle, katika mchezo utakaopigwa Machi 22. Licha ya kuitwa moja ya timu bora England na Ulaya kwa sasa, Arsenal bado inajulikana kwa soka la nidhamu na ufanisi zaidi kuliko burudani. Hata hivyo, hilo halijawazuia mashabiki wao kushangilia kwa nguvu. Kocha Mikel Arteta sasa yuko karibu kuongeza taji lingine kubwa kwenye kabati lake la mafanikio, ikiwa itakuwa ni kombe lake la pili kubwa tangu achukue mikoba ya kuinoa Arsenal, baada ya FA Cup aliyoshinda miaka sita iliyopita. Ndoto ya kutwaa makombe manne msimu huu bado ipo hai kwa Arsenal.