Alichokifanya Trump Huko Venezuela Siyo Kipya; Hizo ndo Tabia za Wababe Wa Dunia Hii!
2026-02-18 - 10:57
Rais wa Marekani, Donald Trump 1. Kwa watu wanaojua historia ya Dunia hii kama akina Hayati Kazilahabi mpaka kuandika vitabu vya “Dunia Uwanja wa Fujo” hili la Trump kumnyakua Maduro siyo jambo jipya. 2. Labda ni jipya kwa wasiojua historia ya Dunia. Na hawa ndo hujichosha kuuliza kwa nini UN iko kimya, China iko kimya, Urusi iko kimya! 3. Sikiliza! Hawa wote ni wale wale. Wametofautiana maeneo ya kufanyia fujo zao tu. Wote ni wababe! 4. Kuna mmoja fujo zake anazifanyia katika utengenezaji wa silaha za maangamizi ili watu wauane yeye apate pesa maana katika mauti kuna ulaji mkubwa! 5. Mwingie fujo zake anazifanyia katika uuzaji wa dawa za kulevya ili watu walewe yeye apate hela maana vilevi ni dili sana! 6. Mwingie fujo zake anazifanyia katika kufadhili ugaidi ili wapate nafasi ya kupora rasilimali za watu apige hela, apate furaha kubwa. Hii inaitwa laana ya rasilimali!; 7. Mwingine fujo zake anazifanyia katika kuua viongozi wanaowapigania maskini ili maskini waendelee kubaki maskini kwa sababu maskini ni mtaji wa tajiri! 8. Mwingine fujo zake anazifanyia kwenye bidhaa feki,dawa feki, kondomu feki, vyakula feki, simu feki, magari feki kwa sababu feki watu wengi huimbilia feki. Ktk feki kuna hela! 9. Mwingine fujo zake anazifanyia kwenye mafuta ili kuitawala dunia kama Henry Kissinger alivyowahi kusema “Control oil and you control nations; control food and you control the people”. 10. Mwingine fujo zake anazifanyia kwenye uharamia wa meli za mizigo kuja Afrika; ili tuendelee kuteseka kwa bei kubwa ya bidhaa! 11. Mwingine fujo zake anazifanyia kwenye uzalishaji wa mbegu za viini tete ukirudia kupanda hazioti ili kuua mbegu zetu na kuendelea kuwapelekea hela! 12. Mwingine fujo zake anafanyia kwenye uzalishaji wa mbolea na sumu za kuua nyasi ili ardhi yetu isiweze kuzalisha tena bila kununua mbolea kwao! 13. Mwingine fujo zake anazifanyia katika kutengeneza magonjwa ya binadamu ili auze dawa na vifaa tiba maana biashara ya dawa inalipa sana! 14. Sasa pale wanapogongana katika fujo zao hali ndo inakuwa mbaya zaidi kwa wanyonge maana kuna kutwangana na kuwekeana vikwazo. 15. Ni sawa na ng’ombe wanapofanya uzinzi nyikani nyasi ndo huumia kwa uzito! Hapa nyasi ni Maduro na wananchi wake; ng’ombe ni ‘China na Marekani! 16. Halafu wakubwa huwa wana namna salama ya kumaliza mambo yao kama walivyoyamaliza wakati waanaigombania Afrika enzi za Scramble for African resources! 18. Waliyamaliza kwa kugawana Afrika kupitia Mkutano wa Berline, kila mtu akapewa shea yake, wakaendelea kuitafuna Afrika kwa huku wenye mali tukiendelea kukodoa macho kama wezi wa kuku! 19. Hii ndiyo dunia ya Uwanja wa Fujo! Mtu akishajiona yeye ni mbabe anaweza kujifanyia chochote bila kujali kitaleta balaa gani kwa watu au la. 20. Si hakuna wa kumgusa? Kwani nani kamgusa Trump mpaka sasa tangu amnyakue Maduro? Atoke wapi. Na hii jeuri kesho anaweza kumvamia mwingine! 21. Hizi ndizo tabia za wababe, kuwaweka wanyonge roho juu. Yaani hii dunia unaweza kulala ni tajiri ukaamka maskini kwa sababu ya jeuri ya mbabe mmoja! 22. Rais Maduro alilala ikulu akaamkia jela, anaishi jela na mke wake, tena uhamishoni. Dunia ina watu wabaya. 23. Nakwambia yamepita majitu katili hapa duniani, Trump wa Maduro akasome. Hivi unamkumbuka Ashurnasirpal II, Mfalme wa Ashuru, aliyetawala Karne ya 9 KK? Huyu mjuba alikuwa shenzi sana. 24. Alivamia nchi za watu na kuwakamata viongozi waliokaidi amri yake na kuwachuna ngozi wakiwa hai na kisha kuwatia kiberiti. 25. Ngozi zao aliziweka hadharani kwenye kuta za miji kama onyo kwa wengine. Hii ndo inaitwa “Kill one, terrify a thousand”, moja ya misemo maarufu ya Sun Tzu katika kitabu chake cha The Art of War. 26. Inamaanisha kutumia adhabu kali kwa mtu mmoja ili kuwatisha wengine wasithubutu! 27. Julius Caesar Mfalme wa Roma alimvamia Vercingetorix, kiongozi wa Wagaul, na kumsafirisha hadi Roma, akamnyonga! 28. Kuna namba nyingine hatari sana. Iliitwa Genghis Khan ya Mongolia Empire. Huyu mshenzi akihitaji mafundi, wasomi, na watu wenye ujuzi iliingia kwenye nchi za watu na kuwachukua kwa nguvu; kiongozi aliyezuia alichinjwa! Loh! 29. Hii imenikumbusha kile kituko cha Ukerewe. Kuna dogo alipigwa na vijana wa hovyo akiwa na demu wake. Dogo alivyofanikiwa kujinasua alitimua mbio akimuacha demu wake, wahuni wakamchukua! 30. Yaani hii dunia,una mali shida, huna mali shida; una hela shida, huna hela shida, ukiwa mbabe shida, ukiwa mnyonge shida; ni dunia ya hofu tu! ****** 1. Mwaka 722 KK Mfalme Hoshea wa Israeli Kaskazini alitekwa na Mfalme Shalmaneser wa Tano wa Dola ya Ashuru kwa kukaidi kulipa kodi! 2. Hapo Israel Kaskazini ndiko yaliishi makabila 10 ya Wana wa Israel yaani Rubeni, Simoni, Dani, Naftali, Gadi, Asheri, Isakari, Zabuloni, Manase na Efraimu. 3. Na makabila mawili ya Wana wa Israel ya Yuda na Benyamini yalikaa Israel Kusini maeneo ya Yerusalemu. 4. Sasa Mfalme Shalmaneser baada ya uvamizi aliondoka na kiongozi wao kwenda kumfunga Ashuru. 5. Kisha alianza kuzingira nchi yao lakini kabla hajamaliza kampeni, aliondolewa madarakani na kufa na Sargon II kushika kiti! 6. Sargon II akawahamisha waisrael wote na kuwachanganya na mataifa mengine huko Ashuru na kupoteza utambulisho wao. Ndiyo maana leo huitwa “Lost Tribes of Israel.” 7. Miaka ya baadaye makabila ya Yuda na Benyamini nao walivamiwa na kupelekwa Babeli 8. Nakumbuka Mfalme wao Zedekia alikaidi kulipa kodi, Nebukadneza Mfalme wa Babeli ndo aiwavamia! 9. Alibomoa Hekalu la Sulemani, ambalo lilikuwa kitovu cha ibada ya Wayahudi. 10. Lakini pia Nebukadreza akaua watoto wa mfalme na kumtoboa macho. 11. Babel ni maeneo ya Baghdad Iraq.Yamebaki mabaki tu. 12. Mpaka hapa nilitaka nikuonyeshe jinsi mbabe mmoja anavyoweza kusabisha tatizo la kudumu! 13. Hawa Wayahudi mpaka leo ni shida tupu. Kila mtu hawataki. 14. Nakumbuka walipotoka Babel mwaka 538 KK, walirudi kama taifa moja lenye mshikamano, wakijenga upya Yerusalemu na hekalu la pili na baadaye wakawa chimbuko la Wayahudi wa leo. 15. Mwaka 135 BK, Warumi waliwafukuza kabisa kutoka Yerusalemu na kuipachika Israel jina jipya: Aelia Capitolina na kutawanyika kote duniani. 16. Kila walikokwenda waliteswa na kufukuzwa kwa sababu ya umoja wao wenye nguvu! Walikuwa na mshikamano uliowapa jeuri ya kusimamia tamaduni zao kuliko kuparamia za wenyeji! 17. Wayahudi wana hadi utamaduni wa kula, hawali kila kitu! Wako very sensitive! 18. Mwaka 1290, walifukuzwa Uingereza kwa madai ya udanganyifu wa kifedha na chuki ya kidini. 19. Ufaransa nayo iliwafukuza mara kadhaa kuanzia mwaka 1306, ikiwalaumu kwa matatizo ya kiuchumi na kidini. 20. Hispania iliwafukuza mwaka 1492 kwa amri ya Ferdinand na Isabella, ikiwalazimisha kubadilika kuwa Wakristo au kuondoka. 21. Ureno ikafuata mwaka 1496 kwa shinikizo la Kanisa Katoliki na Hispania. 22. Italia, hasa Roma na Napoli, Wayahudi walifukuzwa mara kwa mara kati ya karne ya 16 na 18. 23. Poland na Urusi pia waliwabana kuishi katika maeneo maalum (Pale of Settlement) na kufukuzwa mara kwa mara kuanzia karne ya 17 hadi 19. 24. Karne ya 20, Ulaya Mashariki ilishuhudia mashambulizi ya “pogroms” na kilele cha chuki kilikuwa Holocaust, ambapo Wayahudi milioni sita waliuawa. 25. Historia hii ya mateso ndiyo iliyohamasisha harakati ya Zionism na kuundwa kwa taifa la Israel mwaka 1948 kama makazi salama ya Wayahudi. 26. Usumbufu wote huu walisababishiwa na mbabe mmoja aliyeachiwa huru kufanya lolote bila kuguswa. **** 1. Napokwambia duniani wamepita watu wa hovyo sana Trump akasome unatakiwa unielewe. 2. Mtumwa na ng’ombe hawakuwa na tofauti katika treatment. Wote walitreatiwa kama bidhaa tu ya kuuzwa sokoni! 3. Kama wamiliki wa ng’ombe wanavyotumia chuma cha moto kuweka alama kwenye ng’ombe wake ndivyo walivyofanyiwa watumwa. 4. Kilichukuliwa chuma cha motoo na kuchora alama kwenye mwili wa mtumwa kuonyesha yeye ni mali ya mtu tayari imenunuliwa. 5. Habari za mtu si nyau tumeanza kuzisikia siku hizi. Zamani mtu alikuwa nyau kabisa.Soma kitabu cha Slaves in the Family cha Edward Ball, kitukuu cha wamiliki watumwa. 6. Duniani yamepita majibu hatari sana basi tu. Imagine, mtu mmoja anaweza kuamka na kusema nchi kadhaa ziko chini yake, atakayepinga ni kichapo! 7. Mwaka 1823, Rais Monroe wa Marekani, aliaamua kuitangazia dunia kwamba Bara lote la Amerika Kusini na nchi zote za Karebian ni eneo lake la ushawishi, marufuku taifa lolote kutia pua. 8. Hivu unaelewa mtu akisema eneo fulani liko chini ya ushawishi ana maana gani?Anamaanisha mtu huyo anaweza kuwapangia nini cha kufana na nini msifanye; msipotii mtamtambua! 9. Sasa sera hiyo iliyoitwa Monre Doctrine ndiyo inaipa Marekani jeuri ya kuzinyanyasa nchi za ukanda huo Kerebian na Amerika Kusini. 10. Karebiani ni eneo la visiwa na pwani lililoko kati ya Amerika Kaskazini na Amerika Kusini, na magharibi mwa Bahari ya Atlantiki. 11. Eneo hilo lina zaidi ya visiwa 7,000, vikubwa na vidogo vilivyosheheni utajiri wa dunia. 12. Eneo hilo lina jumuisha nchi huru za Cuba, Jamaica, Haiti, Dominican Republic, Trinidad na Tobago, Barbados, Bahamas, Grenada, Saint Lucia, Saint Vincent na Grenadines, Antigua na Barbuda, Dominica, Saint Kitts na Nevis 13. Karibia asilimia 15 ya sukari ya dunia hutoka katika nchi za Caribbean. 14. Na Amerika Kusini ina zaidi ya nchi 12 ikiwa ni pamoja na kila moja Venezuela, Brazil, Argentina, Chile, Uruguay, Paraguay, Bolivia, Peru, Ecuador, Colombia, Guyana, Suriname na French Guiana. 15. Mali zinazopatikana ukanda huu ni pamoja na mafuta (Venezuela, Brazil), gesi asilia (Bolivia), dhahabu, almasi, shaba (Chile), na lithiamu (Argentina, Bolivia, Chile 16. Amerika Kusini ni soko lenye watu zaidi ya milioni 430, na Karebiani zaidi ya milioni 44. 17. Hata msitu mkubwa dunia uko huko. Ni msitu wa Amazon. Unaitwa Mapafu ya Dunia kwa sababu unazalisha oksijeni nyingi duniani. 18. Msitu huo ni mkubwa zaidi duniani, unaokaribia kilomita za mraba 6.7 milioni na uko katika nchi 9 za Brazil, Peru, Colombia, Venezuela, Ecuador, Bolivia, Guyana, Suriname, na French Guiana. 19. Msitu huu una miti zaidi ya bilioni 390, inayochangia kwa kiwango kikubwa katika mzunguko wa oksijeni na kaboni duniani. 20. Pia Baral la Amerika Kusini ilinaongoza kwa uzalishaji wa kahawa duniani, kahawa hiyo inalimwa katika nchi ya (Brazil). 21. Hata mto wenye maji mengi zaidi dunian yaani Amazon River na na jangwa kavu zaidi duniani yaani Atacama viko huko! 22. Sasa unaanza kuelewa kwa nini Marekani walijitangazia ushawishi wa eneo hili na kila aliyekaidi alikipata cha mtema kuni! 23. Kipindi cha Vita Baridi, vitaka kati ya ubepari (Marekani) na ukomunist (Urus ya Kale), Marekani alipiga marufuku nchi za Ukanda huo anaouita nyuma ya nyumba yake kukaribisha ukomunist. Aliyejaribu alichakazwa. 24. Mwaka 1954, Rais Jacobo Árbenz Guzmán wa Guatemala alipinduliwa na vikosi kutoka Honduras kwa msaada wa Rais Dwight D. Eisenhower wa Marekani kwa kosa la kuanzisha ukomunisti na kubinafsisha mashamba ya kampuni ya Kimarekani ya United Fruit Company. 25. Mwaka 1961, Rais John F. Kennedy wa Marekani aliandaa jeshi la watu 1500 kwenda kumpindua Fidel Castro wa Cuba kwa sababu ya kuleta ukomunist ukanda huo wa Karibian, Bahati nzuri Castro, akawawatwanga Marekani na kuua askari 114 na kuteka wengine 1100. Rejea ile vita ya Bay of Pigs. 26. Mwaka 1964, Rais João Goulart wa Brazil alionyesha harufu za kukaribisha ukomunisti nchini kwake kwa kuunga mkono sera za mlango wa kushoto akapinduliwa na jeshi lake kwa msaada wa Rais Lyndon B. Johnson wa Marekani. 27. Mwaka 1973, Rais Salvador Allende,alianza mahusiano na Cuba akapinduliwa na jeshi lake likiongozwa na Augusto Pinochet kwa msaada wa Rais Richard Nixon wa Marekani katika oparesheni Condor. 28. Mwaka 1976 Rais Isabel Perón wa Argentina alizembea kupinga ukomunisti nchini akapinduliwa na Jeshi la Argentina lililoongozwa na Jenerali Jorge Rafael Videla, kwa msaada wa Rais Gerald Ford wa Marekani. 29. Mwaka 1989, Rais Manuel Noriega wa Panama alikamatwa na Rais George H. W. Bush na kupelekwa kufungwa Marekani eti kwa makosa ya biashara ya dawa za kulevya na wakati kosa lake ilikuwa ni kuanzisha ushirikiano na mataifa yaliyokuwa maadui wa Marekani, hasa Cuba na Nicaragua. 30. Mwaka 1998, Hugo Chávez aliingia madarakani na sera ya “Ujamaa wa Karne ya 21”, akabinafsiha mafuta, na kujenga nchi, Marekani wakamuwekea vikwazo. 31. Mwanaume akasema isiwe taabu. Akamuita Mjamaa mwenzake Mchina wapige bizinez za kikubwa na siyo za kulaliana. 32. Kwa wachina, Venezuela ikawa lango la kupenyeza ushawishi wao katika ukanda huo Marekani anaosema ni wake. Eti ni nyuma ya nyumba yake! **** 1. Mchina akaanza kueneza sera zake za miundombinu na uwekezaji yaani Belt and Road Initiative (BRI) katika ukanda huo Amerika na Karebian bila kuogopa. 2. BRI ni mpango wa China wa kuunganisha mabara ya Asia, Ulaya, Afrika, na Amerika Kusini kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu, biashara, na nishati. 3. Inaitwa Silk Road ya Kisasa. Project inajumuisha barabara, reli, bandari, na miradi ya nishati. Zaidi ya 150 nchi zimejiunga na hii project kwa hiari na siyo wenyewe. 4. Tayari China imemwaga zaidi ya dola bilioni 200 katika mradi huo wa kibabe unaotekelezwa duniani kote. 5 Kwahiyo Mchina anapokwamba wanakwenda kuwa superpower ya dunia karne ya 21 unatakiwa umuelewe. Hatanii huyu. Mchina si mtu wa “tuko mbioni!” 6. Kwa Marekani hii ni dharau kubwa. Kwa Mchina huu ni uanamue mkubwa. Hapa ni patamu sana. Hebu ngoja tuone nini kitatokea. 7. Harakati za kumuondoa Hugo madarakani zikaanza! Marekani iliangaza kwamba Chavez ni dikteta na tishio la ukomunisti lakini hawakueleweka. 8. Kila Rais aliyeingia madarakani alijaribu kupambana na Hugo akadunda. 9. Alianza Rais Bill Clinton akashindwa, akaja George W. Bush akashindwa, akaja Baraka Obama akashindwa. 10. Sijui hawakujua kama walikuwa wanapambana na Kanali wa Jeshi? Toka lini Raia akapambana kwa mjeshi akashinda? 11. Hugo mpaka anakufa kwa kansa hakuna kikaragosi kilichomuweza. Alipendwa sana na raia na raia walimbeba sana. Mwaka 2002 Marekani ilipojaribu kumpindua Raia walimrudisha ikulu. 12. Mkanda wenyewe ulikuwa hivi! Mwaka 2002 lilifanyika jaribio la mapinduzi lililodumu siku mbili tu (11 na 13 Aprili). 13. Basi bwana! Tarehe 11 Aprili 2002, maandamano makubwa ya upinzani dhidi ya Chávez yalifanyika Caracas. 14. Viongozi wa juu wa jeshi walimkamata Chávez na kumlazimisha kuandika barua ya kujiuzulu, akagoma. Makanali huwa si wepesi kivileeee! 15. Wafanyabiashara na wapinzani kwa maelekezo ya Marekani wakamteua Pedro Carmona kuwa rais wa mpito huku wafuasi wa Chavez wakiendelea maandamano ya kutaka mwamba arudi! 16 Tarehe 12 Aprili 2002, Rais Carmona akajichanganya kuvunja Bunge a Mahakama Kuu, jambo lililowakera hata washirika wake. 17. Maandamano ya wafuasi wa Chávez yalizidi kuongezeka, yakizunguka Ikulu ya Miraflores. Vikosi vya usalama vilirusha mabomu lakini raia hawakurudi nyuma. 18. Tarehe 13 Aprili 2002, sehemu ya jeshi ikabadilisha msimamo na kuunga mkono maandamano ya wananchi kurejeshwa kwa Chávez Ikulu. 19. Rais Carmona akaona hapa ishakuwa taabu. Akatimkia zake Colombia. Chávez akarudishwa madarakani baada ya saa 47 nje ya ofisi. 20. Wahenga tukagonga cheers kwa kibwagizo cha kwamba UKIWABEBA VIZURI WANANCHI IPO SIKU NAO WATAKUBEBA! Viongozi wenye akili chukueni hiyo! 21. Baada ya Rais Hugo Chávez kurejea madarakani Aprili 2002, alianza kumshambulia Rais George W. Bush mpaka huruma. Kuna siku alimuita Bush Shetani, tukashangaa. 22. Tena ilikuwa kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa mwaka 2006 huko New York Marekani. 23. Siku hiyo Hugo anapanda kuzungumza, jana yake alikuwa amezungumza Rais Bush, basi kabla ya kuanza kuhutubia Hugo akasema, Jana kuna shetani alipita hapa kuzungumza, bado nasikia harufu yake. Shetani huyo alimaanisha Bush! 24. Katika kipindi chake chote cha utawala, Hugozi alifanya biashara ya mafuta na Mchina. Mchina alitema mabilioni ya shilingi, Hugo akayalipa kwa mafupa, Venezuela ikajengwa, wanachi wakala maisha! 25. Mchina kuendelea kunywa mafuta ya Venezuela kilimuuma sana Marekani utadhani yake. Ubabe bhana. Yaani unaumia roho kwa mali za watu. Hugo aliwakimbiza sana mabepari. 26. Marekani wamekuja kupumua baada ya kumuondoa Maduro nmadarakani! Ila Hata kumuondoa Maduro haikuwa kazi ndiyo maana Trump anatamba. 27. Maduro kaichezesha Marekani kwa miaka 13. Aliingia madarakani 19 Aprili 2013 amekuja kuondoka tarehe 3 Januari 2026 kwa ubabe wa Trump na Marekani. 27. Kilichomuumiza Maduro ni vikwazo vya Marekani na washirika wake. Hakuwa na uwezo wa kuvipangua na Mchina hakumsaidia. 28. Nchi ikazorota kabisa kiuchumi. Mwamba akakosa mvuto kwa wanachi. Maandamano na ukandamizaji wa haki za waandamaji yakawa mengi. Siku zake za kuishi ikulu zikaanza kupungua. 29. Nchi yenye hazina kubwa ya mafuta duniani, zaidi ya pipa bilioni 303 inakuwa na uchumi mbovu, hapo ndo ujue dunia hii ina washenzi sana. 30. Ikikukazia unaweza kulala njaa na mali zako. Ni kama Nyerere walivyomsusia kwenye viwanda.Kwanza unajua ilikuaje basi? 31. Nyerere alifungua viwanda vingi chini ya sera ya Ujamaa na Kujitegemea ili kujinasua na makucha ya mabepari, mabepari yakaungana na kumnyima vipuri. Viwanda vikajifia vyenyewe. ****** 1. Kwa picha hiyo niliyokuonyesha hapo kumbe Maduro ilikuwa lazima aondoke tu. Urus, China na Cuba waliishia kumpa tu taarifa za kijasusi kwamba anakwenda kunyakuliwa na siyo kuzuia unyakuo wake. 2. Urusi na China wasingezuia unyakuo wake kwa sababu na wao ni wale wale. Wanapita mule mule kwenye ubabe wa Marekani na Monreoe Docrine yao! 2. Kwa mfano, mwaka 1968, Leonid Brezhnev wa Urus ya Kale na yeye aliibuka na kutangaza Dokrin Brezhnev kuhalalisha kuingilia kijeshi nchi yoyote ya Ulaya Mashariki ambayo ingejaribu kuachana na ukomunisti! 3. Alexander Dubček, kiongozi wa Czechoslovakia, alianzisha mageuzi ya Prague Spring mwaka 1968, akihimiza demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari, na kupunguza udhibiti wa chama cha kikomunisti. Mageuzi hayo yalivunjwa kwa nguvu na uvamizi wa majeshi ya Warsaw Pact yakiongozwa na Urusi. 4. Sasa huyu ndo ungetegemea amkemee Marekani? Anaanzia wapi? 5. Hata baada ya kuvunjika kwa USSR mwaka 1991, mataifa 15 mapya yaliyozaliwa na kuwa huru Urusi iliendelea kuyazuia kuimarisha demokrasia na kujiunga na NATO. 6. Aliyekaidi alitandikwa. Hiki ndicho kinampata Ukraine, kukaidi amri ya Mrusi kujiunga na NATO. Nchi huru kwa nini inanyimwa uhuru wake? Ubabe! 7. Hata hawa Wachina wana sera kama hizo za Monroe na Brezhnev. Sera yao inaitwa Xi Jinping Doctrine hawajaitangaza rasmi lakini ipo. 8. Kupitia sera hiyo, China imeweka wazi kwamba Asia ya Mashariki na Bahari ya Kusini ya China ni ukanda wake wa ushawishi, marufuku taifa lolote kutia pua. Nani kampa hiyo jeuri? Ubabe! 9. Vietnam na Ufilipino walipojaribu kupinga hilo kwa kuomba msaada wa Marekani kulinda uhuru wa Bahari; Mchina ametishia kwa kujenga visiwa bandia na kuweka jeshi. Anawasikilizia. Wamenyweaaa! 10. Sasa huyu ndo wa kumkea Marekani? Thubutuuu! 11. Taiwan ilivyotishia kutaka uhuru na kushirikiana na Marekani; China ilijibu kwa kufanya mazoezi ya kivita karibu na pwani ya Taiwan. Taiwan cheeee! 12.Japan ilipojifanya kukataa madai ya China kumiliki visiwa vya Senkaku na Diaoyu na kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na Marekani kuvilinda visiwa hivyo, Mchina amepeleka meli na ndege za kivita karibu na visiwa hivyo ili mtu atie pua amnyonye. 13. China haimiliki rasmi visiwa hivyo lakini imevishupalia kwa sababu visiwa hivyo vinaweza kuwa na rasilimali za mafuta na gesi. 14. India ilivyopinga ushawishi wa China na kuamua kujiunga na Marekani, Japan, na Australia kupitia umoja wa Quad ili kuzuia nguvu za China katika ukanda wa Bahari ya Hindi na Pasifiki, China aliwapelekea moto, wakazichapa. 15. Hii dunia ni ngumu sana. Kila unapogusa panaunguza. Wababe wanasumbua sana dunia. 16. Hawa ndo wanaososababisha kila mtu aimbe “Januari ngumu, Januari ngumu.” Haya Januari imeisha, unakuja na sound gani tena? 17. Ila Januari bhana! Kila mtu huwa anasomesha hata kama hana mtoto. Januari kila mtu anasema hana hela wakati tunajuwa miaka yote hana hela! 20. Haya maisha ni magumu tu hakuna cha Januari wala nini. Ukatili wa binadamu umetifikisha pabaya. 21. Mwaka 380 KK, Plato alisema mwarobaini wa ukatili wa binadamu ni kumdhibiti, asiwe huru kupitiliza. Anadhibitiwa kwa dola na sheria kali. 22. Plato anasema lazima kuwa na dola itakayoongozwa na watu wenye hekima na maadili ya juu, si wale wanaotawaliwa na tamaa. Watu hawa aliwaita philosopher‐kings. 23. Lakini pia Plato akashauri jamii lazima iwe na mfumo wa elimu na maadili unaodhibiti tamaa za binadamu kama ilivyo kwa Chuo Kikukuu cha Mt. Augustino (SAUT). 24. SAUT wana kozi za Social Ethics na nimeshuhudia baadhi ya viongozi wakubwa nchini waliosoma pale wakifanya vizuri nchini. Hawana tamaa ya madaraka, fedha na ubinafsi. 25. Hawa sasa ndiyo Philosopher’s Kings, viongozi wanaovutiwa na utu kuliko watu; viongozi wanaovutiwa kuona watu wengi wakiwa na furaha, amani na utulivu! 26. Mwisho kabisa, Plato akapendekeza Jamii iwe na Muundo wa makundi matatu ya watu! 27. Kundi la Watawala yaani wanafalsafa; watu wenye sifa zifuatazo; 28. Hekima: Wanatawala kwa kutumia maarifa na uelewa wa kina wa maisha na jamii. 29. *Busara: *Wanafanya maamuzi kwa kuzingatia manufaa ya wengi, si maslahi binafsi. 30. *Maadili: *Wanathamini haki, uadilifu, na uwajibikaji. 31. Uongozi wa kimaono: Wanatazama mbali na kupanga mustakabali wa jamii kwa vizazi vijavyo. 32. Kundi la pili ni Walinzi yaani askari, watu wenye ujasiri na nguvu za kulinda jamii yao. Wako tayari kutoa maisha yao kwa ajili ya usalama wa wengine. 33. Kundi la tatu ni Wazalishaji yaani wafanyabiashara, wakulima, mafundi nk, watu wanaoshughulika na mahitaji ya kila siku. Wanafanya kazi kwa bidii ili jamii iwe na ustawi. 34. Shida inaanzia pale kiongozi anakuwa mfanyabiasha, askari anakuwa mkulima badala ya kulinda nchi na mzalishaji anataka kuwa askari badala ya kwenda kulima na kufanya biashara. 36. Hapa lazima tuwe na jamii ya watu waliochanganyikiwa; jamii iliyojaa uzushi, majungu, uonevu na unyanyasaji. Plato ana hoja. Tumsome vizuri! ***** 1. Pamoja na ushauri mzuri sana wa Plato lakini itoshe kusema kwamba tunaishi katika dunia ambayo uhuru ni ubabe na siyo uungwana tena. 2. Na ubabe uko katika nguvu ya jeshi tu. Masuala mengine ya kiuchumi ukiwa na jeshi imara yanazungumzika tu. 3. Ndiyo maana Adolf Hitler akasisitiza kuwa na uchumi wa kijeshi! 4. Kitendo cha Marekani kuwekeza katika kambi za kijeshi sehemu mbalimbali duniani usidhani ni mjinga. Anajua jeshi imara ndiyo uhuru. 5. Marekani ina takribani kambi 800 za kijeshi duniani, zikiwa zimeenea katika mabara yote, lakini zipo kwa wingi zaidi barani Asia na Ulaya. 6. Nchi zenye kambi nyingi zaidi za kijeshi za Marekani ni Japan (takriban 120), Ujerumani (119), Korea Kusini (73), Guam (54), na Italia (44). 7. Hata hii NATO ni dude la Marekani. Ukipishana na NATO tambua umepisha na Marekani. Jiandae kwa lolote. 8. Leo hii Marekani ana ushawishi mkubwa duniani ndiyo maana akisema anakupiga vikwazo umekwisha. 9. Hivi karibuni Marekani kupitia washirika wake wa NATO wamempiga vikwazo Mrusi kwa sababu ya kuivamia Ukrane! 10. Uchumi wa Urusi ulikuwa unategemea sana biashara na nchi za NATO, hasa kupitia mauzo ya nishati. 11. Kupitia vikwazo hivi mafuta na gesi ya Urusi haiuziki katika nchi hizo tena. Kabla ya vita ya Ukraine takribani asilimia 22.5 ya bajeti ya serikali ya Urusi ilitegemea mauzo ya mafuta na gesi yaliyonunuliwa na wanachama wa NATO. 12. Lakini pia washirika hao wameziondoa benki za Urusi kwenye mfumo wa SWIFT ili kukata mawasiliano ya kifedha na masoko ya kimataifa na kufungia mali za Benki Kuu karibu dola bilioni 300. 13. SWIFT ni kifupi cha Society for Worldwide Interbank Financial Telecommunication. 14. Ilianzishwa mwaka 1973, makao yake Ubeligiji. Kukatwa kwa Urusi kwenye mtandao huu kumeifanya iwe vigumu kushirikiana na masoko ya kimataifa. 15. Lakini pia mabilionea wakubwa kama Abramovich, Usmanov, Sechin na Timchenko waliowekeza katika hizo nchi za NATO mali zao zimetaifishwa zote. 16. Aidha, Urusi imezuiwa kupata teknolojia za hali ya juu kama microchips, mashine za viwanda, programu za kisasa na silaha na vifaa vya kijeshi ili kudhoofisha uwezo wake wa kuendeleza vita vya muda mrefu. 17. Cha kushangaza sasa! Pamoja na vikwazo vyote hivyo, Urusi haijasalimu amri; badala yake imeendelea kuichakaza Ukraine na kuwachosha NATO. Anawatia hasara tu! 18. Urusi imeimarisha ushawishi wake Mashariki ya Kati kupitia Syria kwa kuunga mkono utawala wa Bashar al-Assad. 19. Kwa msaada wa kijeshi na kuweka kambi katika bandari ya Tartus, Urusi imepata nafasi ya kudumu ya kijeshi katika ukanda wa Mediterania. 20. Vilevile, Urusi imejenga ushirikiano wa karibu na Iran. Wamesaini mikataba ya muda mrefu ya ushirikiano wa kiusalama, nishati, na teknolojia. Hapa patachimbika! 21. Ushirikiano huu unawapa nguvu ya pamoja kupinga vikwazo vya Marekani na kuunda mbadala wa masoko ya nishati duniani. 22. Kwa njia hii, Urusi imekuwa na nafasi kubwa katika sera za nishati na usalama wa Mashariki ya Kati. 23. Hii inamaanisha Marekani imepoteza sehemu ya udhibiti wake wa jadi katika eneo hilo. 24. Zaidi ya hayo, Urusi imeunda ushirikiano wa kiuchumi na kijeshi na China, muungano unaopinga ushawishi wa nchi za Magharibi duniani. 25. China kwa sasa inachangia takribani asilimia 25 ya mapato ya bajeti ya Urusi kupitia ununuzi wa mafuta na gesi ya Urusi. 26. Urusi imeendelea kutengeneza na kuboresha silaha zake, ikiongeza uzalishaji wa makombora ya masafa marefu, ndege za kivita, na droni za kivita. 27. Urusi inapata vipuri vya kielektroniki kutoka nchi za Magharibi kwa njia za panya, ikiwemo microchips, sensa, na semiconductors, ambavyo vinatumika katika makombora na droni. 28. Lakini pia, Wagner Group, kundi binafsi la kijeshi la Urusi, linaleta mapato ya kigeni kupitia mikataba ya madini, gesi na mafuta barani Afrika. 29. Hawa jamaa wanafanya kazi za ulinzi wa viongozi, ulinzi wa nchi na misheni nyingine za kijeshi katika nchi mbalimbali duniani. 30. Kundi hili liko katika zaidi ya nchi 15 duniani, hasa Afrika (Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan, Libya). 31. Pia wako Ulaya na Mashariki ya Kati (Ukraine, Syria). Idadi kamili si rahisi kuijua kwa sababu ya usiri mkubwa, siunajua majasusi tena? 32. Jasusi wa kweli kumjua ni kazi ngumu sana, acha hao ambao wakilewa wanajitangaza. Unanijua mie nani? Mie mtu wa mfumo. Bure kabisa! 33. Itoshe kusema hii dunia bila kuwa mbabe utapata taabu sana. Lakini kuwa mbabe ni taabu kubwa zaidi. Hii inaitwa ukimbia nchale, ukisimama nchale! Utajua mwenywe! Simulizi yetu imeishia hapa, tunane kwa simulizi nyingine! 35. Jipatie vitabu vyangu 14 kwa Sh 20,000 softcopy, nakutumia kwa Whatsapp, ukitaka kimoja ni Sh 5,000 tu. Mpesa 0740590451. Ukitaka hardcopy mpigie Bahiri wa Taifa, Patson Chaula, anapatikana kwa namba +255 753 690 907! Vitabu hivi hapa! 1. Kula Chakula Kama Dawa, Epuka Kula Dawa Kama Chakula 2. Malezi:Muandae Mwanao Kuwa na Hadhi Ukubwani 3. Biashara Huanzia Kichwani Si Mfukoni 4. Wasomi Huru Gerezani 5. Maisha ni Kutafuta Si Kutafutana 6. Ukombozi wa Fikra za Mwafrika 7. Fungua Ubongo 8. Miamba ya Afrika 9. Viongozi Walioandika Majina Yao Vibaya 10. Mbinu 16 Alizotumia Yesu Kutoboa 11. Viongozi Wanaoishi Baada ya Kufa 12. Fahamu ya Ndoa Kabla ya Ndoa! 13. Ukombozi wa Fikra 14. Fikra Tunduizi:Tungo za Kufikirisha Cheers Mwl. Denis Mpagaze Muhenga wa Karne ya 21