TheTanzaniaTime

Airtel Divas Watoa Msaada kwa Watoto Wenye Mtindio wa Ubongo Madale

2026-03-16 - 15:48

Dar es Salaam – Wanawake wafanyakazi wa Airtel Tanzania kupitia kundi lao la Airtel Divas wametembelea kituo cha kulea watoto wenye mtindio wa ubongo kinachoendeshwa na Dorcas Foundation kilichopo Madale jijini Dar es Salaam, na kutoa msaada kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho. Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Meneja wa Programu wa Dorcas Home Care, Lisa Mbukilo, amesema kituo hicho kinaendelea kuona maendeleo ya kutia moyo kwa baadhi ya watoto wanaopatiwa huduma za matibabu na uangalizi. Amesema kati ya zaidi ya watoto 70 wanaolelewa kupitia Dorcas Foundation, takribani watoto 20 walioanza kupata huduma katika kituo hicho wameanza kuonesha maendeleo mazuri, ikiwemo uwezo wa kutembea kwa msaada pamoja na kufanya baadhi ya shughuli ndogo za kila siku. Hata hivyo, Mbukilo amebainisha kuwa kituo hicho bado kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa bima za afya, dawa pamoja na vifaa tiba vinavyohitajika kusaidia matibabu na uangalizi wa watoto waliopo kituoni hapo. Kwa upande wake, kiongozi wa msafara wa Airtel Divas kutoka Airtel Tanzania, Jemima Masimba, amesema ziara yao inaonesha dhamira ya wanawake wa Airtel kurudisha kwa jamii kwa kusaidia makundi yenye uhitaji maalum. Amesema kupitia ziara hiyo pia wameungana na wadau wengine katika kampeni ya Kibubu cha Dorcas, inayolenga kuhamasisha michango kwa ajili ya kununua eneo la kudumu litakalotumika kujenga kituo cha kulea watoto wenye mtindio wa ubongo. Naye Mkurugenzi wa Dorcas Foundation, Rehema Semfukwe, amewashukuru wanawake wa Airtel Tanzania kwa kutembelea kituo hicho na kuunga mkono kampeni hiyo. Amesema hatua hiyo itasaidia kupanua huduma na kuwafikia watoto wengi zaidi wenye mahitaji maalum. Mpango wa Airtel Divas unawakutanisha wanawake wafanyakazi wa Airtel Tanzania wanaoshiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii zenye lengo la kusaidia jamii, hususan makundi yenye uhitaji maalum.

Share this post: