Afrika Kusini Yamfukuza Balozi wa Israel, Yampa Saa 72 Kuondoka
2026-01-30 - 16:29
Balozi wa Israel Afrika Kusini, Ariel Seidman Serikali ya Afrika Kusini imempa Balozi wa Israel nchini humo, Ariel Seidman, makataa ya saa 72 kuondoka nchini kwao, kufuatia kile ilichokitaja kuwa ni ukiukwaji wa kanuni za kidiplomasia unaotishia uhuru na heshima ya taifa hilo. Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Idara ya Mambo ya Kigeni ya Afrika Kusini, serikali imesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya kubaini vitendo vya ubalozi wa Israel vinavyokiuka misingi ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa huru. Taarifa hiyo inaeleza kuwa Afrika Kusini inailaumu Israel kwa kutumia mitandao ya kijamii ya ubalozi wake kumshambulia na kumkosoa Rais wa nchi hiyo, Cyril Ramaphosa, kitendo ambacho kimeelezwa kuwa hakikubaliki kwa mujibu wa itifaki za kidiplomasia. Aidha, serikali ya Afrika Kusini imesema ubalozi wa Israel ulishindwa kuijulisha rasmi serikali kuhusu ziara ya maafisa wakuu wa Israel walioingia nchini humo, hali iliyotajwa kuwa ni ukiukwaji wa taratibu za kidiplomasia na kudhoofisha uaminifu katika mahusiano ya kimataifa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vitendo hivyo vinaelezwa kuwa vinakandamiza uhuru wa kidiplomasia wa Afrika Kusini na kuhatarisha misingi ya heshima na mawasiliano ya wazi kati ya mataifa mawili. Kutokana na hayo, Balozi Ariel Seidman amepewa siku tatu kuondoka nchini Afrika Kusini kuanzia tarehe ya kutolewa kwa taarifa hiyo. Uhusiano kati ya Afrika Kusini na Israel umekuwa ukiyumba kwa muda, hususan baada ya Afrika Kusini kuwasilisha shauri dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) mwaka 2023, ikiituhumu Israel kwa kutekeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza madai ambayo Israel imekuwa ikiyakanusha vikali. MRITHI WA UMMY MWALIMU AIBUKA BUNGENI KWA UKALI -“NDOTO IMETIMIA UCHAGUZI HUU 2025 TANGU 2010”